Magufuli Kutoa Laptop kwa kila Mwalimu na Milioni 50 kila Kijiji

code         No comments


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kutoa kompyuta mpakato (laptop) kwa kila mwalimu hapa nchini na shilingi milioni 50 kwa kila kijiji, kwa ajili ya kukuza uchumi endapo kitashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.


Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika mwezi uliopita, ahadi hizo zitatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya mgombea wa chama hicho (2015-2020), John Magufuli. Kwa maana hiyo, mgombea huyo atapaswa kuwaambia Watanzania maneno hayo wakati wa kampeni.

Magufuli atakabidhiwa ilani hiyo wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) uliopangwa kufanyika mjini Dodoma kati ya Agosti 12 na 13 mwaka huu, mjini Dodoma.

Hatua hiyo ya CCM kutoa laptop kwa walimu ni tofauti na ilivyozoeleka katika nchi nyingine kama Kenya na Rwanda ambako serikali zake zinatoa kompyuta hizo kwa wanafunzi.

Raia Mwema limeambiwa na vyanzo vyake kuwa mpango wa kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji hapa nchini una lengo la kupunguza tatizo la ajira na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati Maalumu iliyotengeneza ilani ya chama hicho kwa ajili ya kipindi cha mwaka 2015-2020, January Makamba, alilithibitishia gazeti hili Jumatatu wiki hii, kuwa ilani ya CCM iko tayari na imezungumzia mambo mengi ya msingi yakiwamo hayo aliyoulizwa na gazeti hili.

“Ilani iko tayari na mgombea atakabidhiwa kwenye mkutano ujao wa NEC. Siwezi kusema mengi kuhusu hiyo ilani lakini naweza kukuhakikishia kwamba ni ya kisasa, kibunifu na inayokidhi mahitaji ya sasa ya taifa letu,” alisema.

Akieleza kuhusu kompyuta mpakato hizo, January alisema zitakuwa na uwezo wa kutumia nishati ya jua (solar) ili kuwafanya walimu waliokuwepo kwenye maeneo yenye shida ya umeme kuweza kuzitumia pasipo shaka.

“Ilani hii imezingatia mazingira ya nchi yetu kuwa kuna maeneo ambako umeme ni tatizo. Hivyo kompyuta hizo zitakuwa na uwezo wa kutumia nishati hiyo ili walimu waweze kuzitumia mara zote.

“Pia, kompyuta hizo zitakuwa zimewekwa kabisa vitabu na mambo mengine ya kusaidia walimu kufundisha hivyo hawatakuwa wanapewa mashine pekee bali na vifaa vingine vya kazi,” alisema Makamba.

January alisema kompyuta hizo zitagawiwa kwa walimu wote waliopo nchini na kuwa CCM imeona ni vema walimu kwanza wakawezeshwa kiteknolojia kabla ya kuelekea kwa wanafunzi kwenye awamu nyingine.

“Tunafahamu ziko nchi ambazo wameamua kuanza na wanafunzi. Sisi tumeona tuanze na walimu kwanza ili iwe rahisi kwao kuwafundisha wanafunzi wakati CCM itakapoanza mpango maalumu kwa watoto,” alisema Makamba.

Mbali na January, wajumbe wengine wa kamati hiyo ya wataalamu iliyoongozwa na Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wasira, walikuwa ni Anamringi Macha (Katibu), Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali-Zanzibar, Ali Juma Shamhuna.

Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Anthony Mavunde, Mbunge wa Manyoni Mashariki, Kapteni (mstaafu) John Chiligati na Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Aboud.
Kuhusu suala la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji, Makamba alisema fedha hizo zitatolewa katika kipindi cha miaka hiyo mitano na zitakuwa za mzunguko ili kusaidia watu wengi zaidi kufaidika.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina takribani vijiji 19,200 na kama serikali itatoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji, maana yake ni kuwa itahitaji kuwa na kiasi cha shilingi bilioni 900 katika muda huo.

January alisema mtindo na utaratibu utakaotumika kwa ajili ya kutoa fedha hizo za uwezeshaji vijijini utaelezwa na kufafanuliwa vizuri wakati kampeni zitakapoanza rasmi.
Lowassa na Magufuli

Makamba ambaye pia alijitokeza kuwania urais kupitia CCM katika kinyang’anyiro cha ndani ya chama, alisema chama tawala hakina hofu na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, ambaye atashindana na Magufuli kuwania urais; yeye akitumia tiketi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumza kwa kujiamini, Makamba alisema kinachoonekana katika matukio ya karibuni ya Lowassa ni sawa na uigizaji na hivyo wao CCM hawana sababu ya kuhofia chochote.
“Sisi katika chama tunaamini kuwa kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere angekuwa hai leo na kungekuwa na wagombea hawa wawili; Lowassa na Magufuli, bila shaka angemchagua John Pombe Magufuli. Hili halina shaka.

“Mgombea wetu Magufuli anauzika. Ilani yetu mpya imejaa mambo makubwa mapya yatakayotoa matumaini kwa mamilioni ya Watanzania ambao wana imani kubwa na Chama Cha Mapinduzi pamoja na mgombea wake.

“Tutafanya kampeni ya nyumba kwa nyumba. Si tu ya maandamano na mikutano ya hadhara. Mtandao wa kufanya hivyo tunao na hatubahatishi. Sijui wenzetu wana ilani gani lakini yetu iko tayari na wakati utakapofika tutawaeleza wananchi kila kitu na nukta hadi nukta,” alisema.
Maandalizi ya Ilani

Ukiondoa CCM, vyama vingine viwili; ACT Wazalendo na Alliance for Democratic Change (ADC) ndivyo pekee ambavyo hadi vimekamilisha mchakato wa uandaaji wa ilani za uchaguzi.

Hadi sasa, haijafahamika kama mgombea urais wa Ukawa, Lowassa, atatumia ilani ya uchaguzi ya Chadema alichojiunga nacho au umoja huo utatengeneza ilani inayojumuisha mawazo na matamanio ya vyama vyote vinne vinavyounda umoja huo.

Vyama hivyo ni Chadema, NCCR Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy (NLD)


chanzo:www.raiamwema.co.tz


Published by code

Nulla sagittis convallis arcu. Sed sed nunc. Curabitur consequat. Quisque metus enim venenatis fermentum mollis. Duis vulputate elit in elit. Si vous n'avez pas eu la chance de prendre dans tous.
Follow us Google+.

0 comments:

© 2014 punguzo . Designed by Bloggertheme9
Powered by Blogger.