SIKU chache baada ya uongozi wa NLD mkoani Mtwara kudai hautambui mpango wa kuachiana majimbo unaohubiriwa na viongozi wakuu wa umoja wa vyama vinne vya upinzani, hali si shwari katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, baada ya Chadema na CUF, kila kimoja kusimamisha mgombea wake jimboni humo.
Hali hiyo iliyojitokeza jana baada ya mgombea wa Chadema, David Lugakingira kuchukua fomu kuwania ubunge wa jimbo hilo, juzi asubuhi ilhali ikielezwa CUF ndio waliokuwa wamepewa baraka na umoja wa wapinzani maarufu kama Ukawa.
Saa chache baada ya Lugakingira, mgombea wa ubunge wa CUF, Salama Omary Awadh naye alifika na kupatiwa fomu za kugombea ubunge katika jimbo hilo.
Ingawa viongozi wa CUF wilaya ya Morogoro Vijijini, walisema kuwa katika mgawanyo wa Ukawa, jimbo hilo limetolewa kwa CUF, ndiyo maana walimuandaa mgombea huyo waliyefuatana naye kwenda Ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro na kushuhudia mwenzao wa Chadema amechukua fomu kwa jimbo hilo.
Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Morogoro inashughulikia majimbo mawili, ambayo ni Morogoro Kusini na jingine Morogoro Kusini Mashariki .
Katika daftari la Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo pia lilikutwa jina Lugakingira wa Chadema, akiwa tayari amekabidhiwa fomu ya kugombea ubunge na wasimamizi wasaidizi wa jimbo na kuleta taharuki kwa upande wa CUF.
Kabla ya kumkabidhi fomu mgombea wa CUF wa jimbo hilo, Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi wa jimbo, Mary Kayona , alimtaka kuonesha barua rasmi iliyosainiwa na kugongwa mhuri na uongozi wa chama chake kilichomteua na mgombea huyo kuitoa na kusomwa na msimamizi huyo mbele ya viongozi wa chama hicho.
“Kabla ya kukukabidhi fomu hizi, tunahitaji tupate barua ya uthibitisho wa kuteuliwa na chama chako...alisema Kayona kwa mgombea huyo wa CUF aliyefuatana na viongozi wa chama na wanachama wengine."
Msimamizi Msaidizi baada ya kuisoma barua hiyo na kusaini katika kitabu cha kumbukumbu alimpatia vitabu vya sheria ya uchaguzi mgombea pamoja na fomu za kujaza kulingana na kanuni na sheria ya uchaguzi inavyoelekeza.
Naye Msimamizi Msaidizi wa Jimbo, Charles Gunewe, alisema, wanao wajibu wa kutoa fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa wagombea wa ubunge wanaothibitishwa kwa barua kutoka katika vyama vyao na ndiyo maana kila mgombea anapatiwa fomu hizo kulingana na sharti hilo .
Alisema , zoezi la utoaji wa fomu limeanza tangu Agosti Mosi, mwaka huu ambapo hadi kufikia Agosti 15, mwaka huu vyama vitano tayari wagombea wake wamechukua fomu za kuwania ubunge katika majimbo hayo mawili.
Alivitaja vyama hivyo ni Chama cha Jahazi Asilia, Chama cha Wakulima (AFP), TLP kimesimamisha kwa majimbo yote mawili , ambapo Morogoro Kusini mgombea wake ni Noge Mwegalawa.
Vyama vingine ni Chadema wilaya ya Morogoro Vijijini Kichama kimemsimamisha Lugakingira aliyechukua fomu ya kugombea ubunge katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki.
chanzo cha habari :www.habarileo.co.tz
chanzo cha habari :www.habarileo.co.tz
0 comments: