Hali tete UKAWA ni baada ya Lipumba kung'atuka

code         No comments

SASA ni dhahiri kuwa kumkaribisha na kuteuliwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa Mgombea Urais wa Umoja unaoundwa na vyama vinne vya upinzani (Ukawa), umeleta mgawanyiko ambao umemlazimu Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (63), kujiuzulu wadhifa huo.
Mara baada ya Lowassa kukaribishwa na Ukawa Julai 28, mwaka huu, na siku iliyofuata kujitoa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mpasuko ulianzia ndani ya umoja huo. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alianza kutoonekana katika matukio makubwa yaliyohusu ujio wa Lowassa ndani ya chama hicho na Ukawa kwa ujumla.
Badala yake, Profesa Lipumba na wenyeviti wenzake wenza wa Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Dk Emmanuel Makaidi wakawa ndio vinara katika kumpokea na kumteua Lowassa kuwa mgombea wao wa urais. Dk Slaa akapotea machoni mwa Watanzania, na wakati Lowassa alipoteuliwa kuwa mgombea wa urais, Jumanne wiki hii, Profesa Lipumba akakosekana katika shughuli hiyo muhimu na hatimaye zikaibuka taarifa kuwa amejiuzulu.
Juzi, alibanwa na wanachama CUF waliokusanyika kwenye Makao Makuu Buguruni Dar es Salaam, wakitaka kufahamu hatma ya taarifa za kujiuzulu kwake, lakini akatoka ofisini kwake na kuwaeleza kuwa “chama ni taasisi na sio mtu mmoja.” Lakini jana, profesa huyo maarufu wa uchumi ndani na nje ya Tanzania, alivunja ukimya huo kwa kutangaza kujiuzulu Uenyekiti wa CUF Taifa kuanzia jana.
“Nimeamua kwa ridhaa yangu kuachia madaraka rasmi ndani ya CUF, nitabaki mwanachama wa kawaida, dhamira yangu inanisuta. Tumechukua watu waliotoka CCM ambao waliipinga Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Jaji Warioba,” Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano aliouitisha.
“Sijashawishiwa na mtu wala kikundi, ni dhamira yangu inanisuta, mimi ndiye mwanzilishi wa Ukawa, sasa tumewapokea wanasiasa waliotoka CCM, tumeshindwa kuenzi na kuzingatia maamuzi yetu kwenye vikao vya Ukawa,” aliongeza.
Alisema ameamua kujiuzulu kwa sababu ya mambo makuu mawili; moja ni Ukawa kukubali kupokea waliotoka CCM ambao walikuwa kikwazo kwenye Bunge la Katiba, na pili ni CUF kutothamini mchango wake na hivyo kuonekana yeye ni kikwazo. Uamuzi wa Profesa Lipumba umetegua kitendawili cha siku kadhaa kwa wanachama na viongozi wa CUF kuhusu taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari vikisema ameamua kuachana na wadhifa huo.
Aidha, kujiuzulu kwake sasa kunaifanya CUF katika muda mfupi kupoteza viongozi wawili wa juu; Mwenyekiti Profesa Lipumba na Makamu Mwenyekiti wake Zanzibar, Juma Duni Haji aliyejitoa na kujiunga na Chadema ambako ameteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa Lowassa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Profesa Lipumba alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF kuanzia mwaka 1999, akachaguliwa tena mwaka 2004, 2009 na 20014. Ameshiriki kuwania urais katika chaguzi zote za vyama vingi kuanzia 1995 akishika nafasi ya pili, 2000 wa tatu, 2005 wa pili na 2010 wa tatu.
Profesa Lipumba alisema baada ya kujiuzulu, atajikita kufanya utafiti wa uchumi na kutoa ushauri wa maendeleo ya uchumi shirikishi kwa taifa ili nchi ikusanye mapato ya serikali na kufikia asilimia 20 ya Pato la Taifa. Katika taarifa aliyoisoma mbele ya waandishi wa habari, alisema alishaiarifu Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF Agosti Mosi mwaka huu kuhusu uamuzi wake.
Kwa mujibu wake, aliwaambia anafanya hivyo baada ya kukamilisha taratibu za ushirikiano ndani ya Ukawa na ameshakabidhi barua ya kung’atuka kwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa CUF, lakini ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida na kadi yake ya uanachama ameilipia hadi mwaka 2020.
Akizungumzia kwa undani kuhusu uamuzi huo, alisema mambo mengine ya chama atayazungumza siku zijazo, na kwamba wakati wote akiwa ndani ya CUF, alijitahidi kujenga chama na amepitia misukosuko mingi hadi kuwekwa gerezani.
“Nilijitahidi kujenga chama, na nilishtakiwa na kesi bado inaendelea kwa madai ya kufanya vitendo vya uhalifu na kufanya maandamano yasiyo halali, lakini hayo yote yalikuwa ni kuhakikisha chama kinakuwa imara,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema hakuwa na nia ya kugombea Uenyekiti wa CUF mwaka 2014, lakini mchakato wa kupata Katiba Mpya ulimsukuma kuendelea na uongozi kwani ulikuwa muhimu. Hivyo, akiwa ndani ya Bunge la Katiba, ndio kulianzishwa Ukawa kwa lengo la kutetea na kuheshimu maoni ya wananchi yaliyoratibiwa na iliyokuwa Tume ya Jaji Warioba.

Published by code

Nulla sagittis convallis arcu. Sed sed nunc. Curabitur consequat. Quisque metus enim venenatis fermentum mollis. Duis vulputate elit in elit. Si vous n'avez pas eu la chance de prendre dans tous.
Follow us Google+.

0 comments:

© 2014 punguzo . Designed by Bloggertheme9
Powered by Blogger.